MTOTO HUFANYA ZAIDI KILE UNACHOKIFANYA KULIKO KILE UNACHOMWAMBIA AFANYE.
Siku moja nikiwa nimepumzika nyumbani baada ya kutoka kazini, watoto wadogo kadhaa wenye umri kati ya miaka 3 - 5 walikuwa wakicheza jirani na mimi. Nilishuhudia tukio lililonifadhaisha kiasi cha kupigwa na butwaa. Katika kucheza kwao, mmoja kati ya wale watoto alimkaripia mwenziwe kwa kusema "Sara mbwa wewe! Sara mbwa wewe! Sara mbwa wewe!" Katika mshituko wangu niliwazingatia watoto wale nikitaka kufahamu sababu iliyomfanya huyu msichana mdogo kumtukana mwenzake.
Baada kuchunguza, nikagundua kuwa huyu Sara alikuwa amechukua kikopo cha mwenzake bila ridhaa ya mwenye kikopo. Lakini nikajiuliza, hivi kweli kitendo hiki tu ndiyo sababu ya kumfanya msichana mdogo kiasi hiki kumtukana mwenzake kwa jazba kiasi kubwa namna ile? Jawabu nililolipata likanifikirisha juu ya wazazi wa mtoto yule aliyetukana. Kwa kweli mama wa mtoto yule nilimfahamu. Mara kwa mara nimekuwa nikimsikia akimtukana mtoto wake tusi lile lile lililotumiwa na mtoto kule mchezoni. Hapa ndipo inapokuja funzo muhimu katika malezi.
Watoto wana kawaida ya kufanya vile tunavyofanya sisi zaidi kuliko vile tunavyowaambia wafanye. Kizazi tunachokilea kiko katika hatari ya kushindwa kusikia na kutii maonyo kwa sababu wazazi wengi hawatendi vile wanavyowaelekeza watoto wao watende. Unaweza kusema kuwa "Yeye ni mtoto, sasa mimi ntafanyaje mambo ya kitoto ili aige?" Ndugu zangu, malezi ni uwekezaji, ukiwekeza kwa mtoto angali bado mdogo utakuwa umeokoa muda wa kukimbizana naye vichochoroni pindi atakapokuwa kijana.
Hatari iliyopo hivi sasa ni kwamba vijana wengi wanapata watoto wakiwa wangali vijana, hivyo bado wanakuwa na hamu ya kuendelea kula ujana. (Ninaposema vijana hapa, ninamaanisha vijana wa kiume na wa kike pia). Kijana, jambo unalopaswa kulifahamu kuanzia leo ni kwamba, unapopata hadhi ya kuitwa baba au mama, yapo mambo ambayo hupaswi kuyafanya au kujihusisha nayo tena ili kuhakikisha mtoto wako anadumu kukuona wewe kama role model wake.
Tunaishi katika zama ambazo "Ulimwengu una uwezo mkubwa wa kufunza watoto wetu kuliko wazazi". Lakini kwa nini iwe hivyo? Kama unayo tabia ambayo unadhani mtoto wako akiwa nayo hutapendezwa, ni vyema ukaiacha. Hata kama kuiacha ni jambo gumu basi jaribu kuificha ili asiishuhudie kwa macho yake ikiwa kwako. Jizuie tu kuleta wanawake au wajomba usiku mtoto akiwa amelala. Jizuie tu kuvuta sigara mbele ya mtoto. Jizuie tu kuonekana umelewa mbele ya mtoto na mambo mengine kama hayo.
Ni rahisi sana kumkanya mtoto dhidi ya kutukana kama wewe si mtukanaji. Hebu fikiria mzazi wa mtoto mtukanaji hapo juu, anaweza kweli kumkanya mwanawe asitukane na akafanikiwa!? Watoto ni zawadi ya pekee tuliyopewa na M/Mungu. Kila aliyepewa mtoto Mungu amempa maagizo kuwa "Ninakupa mtoto huyu, umlee badala yangu". Kwa hiyo hata kama tunaishi katika dunia iliyoharibiwa, isiwe sababu ya sisi kuisaidia kuharibu watoto wetu.
Massatu