UKIFANYA KAMA HUJALI, HUTASUMBUKA!
KUNA kelele nyingi sana kutoka kwa akina mama, wakilia kutendwa na wenza wao. Nimewahi kukutana nao wengi sana, wakilalamika na ukijaribu tu kuwagusia kuhusu nia yako ya kutaka urafiki nao, utawasikia: “Weee, tena sitaki hata kumsikia mtu anaitwa mwanaume.” Na unapotaka kujua kulikoni, atakupa simulizi ndefu juu ya uhusiano wake wa kimapenzi ulivyokatishwa ghafla na mwenza wake kutokana na sababu mbalimbali, lakini kubwa huwa ni kukosa uaminifu.
Ninataka kuwapa siri, siyo tu wanawake, bali hata wanaume.Wakati mwingine tunajiumiza mioyo yetu sisi wenyewe, kwa sababu tunatumia muda mwingi kujipa mawazo ambayo yanatuondolea furaha tunayopaswa kuwa nayo kwa muda mwingi.
Kufikiri sana kuhusu mwenza wako ni ugonjwa ambao mwenye uwezo wa kuutibu siyo mwingine zaidi yako. Na ugonjwa huo unatokana na kosa ambalo wewe ulilifanya siku ile ya kwanza ulipoamua kuanzisha uhusiano wa kimapenzi naye.
Kuna wanawake wanasema wanaume ni waongo sana, kwamba watakudanganya kwa maneno matamu, lakini wakishakupata wanabadilika. Huwa napinga sana msemo huu, siyo kwa sababu mimi ni mwanaume, bali kwa sababu hayana ukweli wowote.
Wanaume siyo waongo isipokuwa hivi ndivyo tulivyoumbwa. Mungu alimfanya mwanaume ampate mwanamke kwa vishawishi, ndiyo maana wanaojaribu kutumia nguvu sheria inawakabili. Vishawishi hivi viliumbwa, tatizo huwa jinsi gani mwanamke anavyovipokea!Hata wewe mdada, mwanaume anapokusimamisha njiani, anapoanza kukusemesha mkiwa garini au popote pale, unajua kabisa huyu sasa anaanza kubwaga sera, unajua kabisa atakushawishi ili ukubaliane naye hatimaye uwe wake.
Kwa maana hiyo, wakati unamsikiliza, akilini mwako unajua kama anafanana na anachokisema au la. Ndiyo, kuna watu wanafanana na wengine hawafanani kabisa. Kwa mfano, mtu atakuambiaje atakununulia gari wakati mmekutana kwenye daladala?
Maana yangu ni kuwa unaweza kumkubali mwanaume siyo kwa sababu ya kuamini anachokisema, bali kwa vile tu, wewe mwenyewe umevutiwa naye pia. Kwani uongo, hata wanawake nao si wanapenda kama wanaume walivyo?
Siku ya kwanza ya kumsikiliza, unakuwa pia umeshamuelewa. Unapomkubali, maana yake ni kuwa uko tayari kwa lolote, hasa baya. Niwape angalizo, mara zote fikiria sana kuhusu kutendwa kuliko mazuri, kwa sababu ukishajiweka tayari kiakili kwa jambo hilo kutokea wakati wowote, wala hutapata taabu.
Na tena, namna nzuri ya kujiweka mbali na stress za kutendwa, wewe ni kujifanya kutojali. Ukiona siku hizi amebadilika, kama alikuwa mtu wa kukupigia simu kila saa na sasa anapiga mara mbili au tatu tu kwa siku, uchune!
Ukiona labda amepunguza mashamsham, muulize maana huenda kweli umemkera, lakini akijifanya kutingisha kichwa na kuendelea na shughuli zake, achana naye.
Amini nakuambia, atakapokuona huna presha, mwenyewe atajishtukia, atajiuliza, mbona huyu siku hizi kama hana habari vile, ana mtu nini? Utashangaa kuona yeye ndiyo anakuja kwako na kulalamika kuwa siku hizi umebadilika!
Lakini nirudie tena kuwaasa, kuweni waangalifu sana siku ya kwanza mnayokata shauri la kushiriki mapenzi na mtu, ndiyo siku inayoshikilia matumaini yako ya baadaye, ni bora kusubiri kuliko kuharakia karaha!VIA/irenemwamfupejamii.blogspot.com