VITA UNAVYOPITIA MAISHANI VINAKUIMARISHA. USIOGOPE!


🔴Mpendwa naomba nikutie moyo katika vita unavyopitia maishani. Mungu ameruhusu hivyo vita maana anajua njia ya pekee ya wewe kuendelea kuimarika katika maisha yako ya imani na mahusiano yako na Yeye ni kwa njia ya hivyo vita na hizo changamoto unazopitia maishani.
🔴Kumbuka siku zote uwapo vitani, haijalishi hiyo vita ni kubwa kiasi gani, si kubwa ukilinganisha na vita vilivyo mbele yako katika siku za usoni. Vita vya jana vinakuandaa kwa ajili ya vita vya leo na kadhalika vita vya leo vinakuandaa kwa ajili ya vita vya kesho.
🔴Wakati Daudi akiwa peke yake kule nyikani na kondoo za baba yake, alitokewa na dubu na simba. Daudi angeweza kukimbia maana kw a kweli ukilinganisha dubu na simba na Daudi, Daudi asingekuwa kabisa na uwezo kwa namna ya kawaida kukabiliana nao. Lakini Daudi katika ushuhuda wake kwa Sauli alisema kuwa Mungu alimwokoa na kinywa na makucha ya Dubu na Simba.Ushuhuda wa vita vyake vya jana vilikuwa kianzio vya vita vyake vya leo. Daudi aliandaliwa na vita vyake dhidi ya dubu na simba kukabiliana na Goliati maana Mungu aliyemwona alipokabiliana na dubu na simba alikuwa na uhakika kabisa kuwa ni Mungu atakayemwona atakapokabiliana na Goliati.
🔴Usidharau vita vyako vya leo maana vinakuandaa kwa ajili ya vita kubwa zaidi kesho. Mungu anaikuza imani yako kupitia vita vyako vya leo ili iwe imara vya kutosha kwa ajili ya vita vyako vya kesho.
🔸Usikubali kunyong’onyeshwa na pito lolote la leo.
🔸Chukulia kama ni maandalizi kwa ajili ya mapito makubwa zaidi kesho.
🔸Endelea kumwamini Mungu katika lile ulipitialo leo.
🔸Katikati ya vita unavyopitia ukihakikisha haya unayafanya kwa uaminifu na nidhamu ya hali ya juu utu wako wa ndani utazidi kuimarishwa katika hali hiyo unayopitia.
🔴Kwa hiyo hatulegei; bali ijapokuwa utu wetu wa nje unachakaa, lakini utu wetu wa ndani unafanywa upya siku kwa siku. Maana dhiki yetu nyepesi, iliyo ya muda wa kitambo tu, yatufanyia utukufu wa milele uzidio kuwa mwingi sana; tusiviangalie vinavyoonekana, bali visivyoonekana. Kwa maana vinavyoonekana ni vya muda tu; bali visivyoonekana ni vya milele.
+3

DOWNLOAD APP YETU GOOGLE PLAY BONYEZA HAPA

DOWNLOAD APP YETU GOOGLE PLAY BONYEZA HAPA