KWA KIWANGO GANI MAKOSA YAKO YANAATHIRI MAHUSIANO YAKO?
Fans, Alhamis njema
Tafakari yetu leo inahusu jinsi ya kutatua matatizo
1. Umeshawahi kumuomba mtu kitu halafu yeye akakuahidi vizuri ila asikutimizie, na wala asikuambie kuwa haiwezekani bali kwa namna mambo yanavyoenda tuu utajua kuwa mtu huyo hatokusaidia.
2. Je umewahi kumdai mtu ikafikia mahali ukimtafuta kwa simu hapokei , hapatikani au simu inakatwa, anazima, ukimuandikia message hajibu, na emails zako ndio kazichunia kabisa.
Basi sikiliza:
Matendo hayo hapo na yanayofanana na hayo yanasababishwa na kasumba ya watu kudhani kulikimbia tatizo ni kulitatua. Wengi wanaogopa kukabiliana na tatizo, kujadili na yule ambaye wanadhani wamemkosea au tuseme yule ambaye ataumia au ameumia kutokana na maamuzi yao.
Unapodaiwa halafu ukaanza kuzima simu, kutokujibu message au kutokata kuonana na anayekudai yawezekana kabisa ukawa upo katika ugonjwa huu. Unaogopa kujadiliana, unaogopa kuli-face tatizo.
Kumbuka kwa namna hii hautatui tatizo, bali ndio kwanza unaliongeza kwani unaharibu mahusiano yako na mtu husika, unajipotezea amani ya moyo na unausonga ubongo wako kwa mambo “magumu” hivyo kuunyima uhuru wa kufikiri vema.
Kasumba hii huanza kidogo kidogo kwa mambo madogo madogo, mpaka unajikuta hata kwa mambo makubwa unakuwa muoga. Pengine ni malezi uliyokulia ambapo haukupewa nafasi ya kujieleza, ulitakiwa tuu kufuata unayoambiwa, na ilikubidi kupinga kwa namna yako isiyo ya wazi wazi, mfano ulipotumwa kuenda kufanya shughuli fulani wakati wewe ulitaka kufanya shughuli nyingi , ukiwa mdogo uliamua kukubali kwenda hata hivyo, hukufanya kama ulivyoambiwa badala yake ukaishia kucheza.
Hata ukiwa mkubwa inaendelea kwa mfano unajua wazi kuwa hata hautoweza kufika kwa wakati katika ahadi mnayokubaliana ila unajikuta unakubali tuu kwa kuwa unaogopa kujadili kutokuweza kwako. Unadhani hapo unatatua tatizo kumbe ndio kwanza unalizidisha.
Mojawapo ya mbinu za kushinda hili ni :
Kuamini kuwa ni busara zaidi kujenga mahusiano mema na watu kuliko kuogopa kuonekana umekosea au kuliko kudhani utamuumiza mtu kwa kusema ukweli, kumbe tambua ataumia zaidi akijua umemdanganya kuliko unavyodhani eti ataumia kwa ukweli wako.
Usiogope hata kama umekosea. Hakuna aliyemkamilifu hapa duniani. Kama ulitaraji kwa dhati kufanya jambo fulani ila mazingira au udhaifu wako ulikufanya ushindwe kutimiza ulichotakiwa kufanya ni vema ukajielezea. Itakuletea heshima zaidi, na kukupa nafasi ya kufanya makubwa zaidi.