Ya kuzingatia unapokutana kwa mara ya kwanza na mpenzi wako!

 





Mada ya leo hii ni maalum kwa wale wanaoanzisha uhusiano mpya au wale wanaoingia kwenye uhusiano wa kimapenzi kwa mara ya kwanza. 


Yawezekana ukawa ‘umemtokea’ mtu na kumueleza kwamba unampenda na kwa bahati nzuri jibu likawa zuri kwa yeye kukukubalia ombi lako. 

Kuna ile siku ya kwanza ambayo mnapanga mkutane ili muweze kuzungumza mambo kadha wa kadha kuhusu uhusiano wenu.

Siku ambayo mnakutana kwa mara ya kwanza ni siku muhimu sana kwenu, ni siku ambayo kila mmoja anatakiwa kuwa makini. Achilia mbali hayo, yapo mambo unayotakiwa kuyazingatia ili kuifanya siku hiyo iweze kuwa ya kihistoria. 
Haya ndiyo ambayo leo hii nimedhamiria kuwaandikia angalau kwa ufupi nikiamini kwamba, yatakuwa ni yenye manufaa kwenu.

Mazungumzo yenu

Huyu mpenzi wako ndiyo mnakutana kwa mara ya kwanza, jitahidi sana mazungumzo yako yawe ya kumfanya ahisi amempata mtu sahihi katika maisha yake. Kuwa makini na kila neno na kila sentensi inayotoka kinywani mwako. 

Usijioneshe kwamba wewe ni mzungumzaji sana wala mkimya sana. Kuwa katikati kwa sababu, kuongea sana au kuwa mkimya sana ni tatizo linaloweza kuuyumbisha uhusiano wenu kwa siku za mwanzo.

Zungumzia mambo yanayogusa maisha yenu na siyo kuhusu watu wengine. Andaa mada kichwani mwako ambazo ungependa mzizungumzie mtakapokutana. 

Itakuwa ni kitu cha ajabu sana endapo utaanza kuuliza ‘Hivi ulishakuwa na uhusiano na watu wangapi mpaka sasa?’ Swali hilo si la msingi sana kuliuliza kwa siku hiyo kwani linaweza kuyumbisha pia uamuzi uliouchukua wa kumkubali. Dadisi mambo ya msingi tu na mengine yapotezee.

Utoke vipi?

Suala la kuchagua nguo za kuvaa pale unapokwenda kukutana na mpenzi wako kwa mara ya kwanza si la kupuuza. Wapo watakaosema suala la mavazi halina umuhimu bali mapenzi hutoka moyoni, ni sawa lakini kuvaa kwako pia kunaweza kumfanya mpenzi wako avutiwe nawe zaidi.

Sisemi kwamba kama hauna nguo na viatu vizuri ukaazime, hapana! Chagua katika hizo hizo ulizonazo zile ambazo unaamini kabisa zitaongeza upendo kutoka kwake.

Pia vaa kulingana na wakati na sehemu mnayokwenda. Kama ulisoma moja ya makala zangu nilizowahi kuandika huko nyuma yenye kichwa cha habari kisemacho “Uvae vipi unapokwenda wapi, utakuwa unafahamu unachotakiwa kufanya.

Aidha, kama ni mwanamke usijirembe kupitiliza, jipulize manukato yasiyoweza kumkera mpenzi wako tena iwe kwa mbali sana. Kwa kifupi muonekano wako uwe ‘simpo’.

Muende wapi?

Maeneo ambayo mara nyingi sana wapenzi hupenda kukutana ni ufukweni, hotelini, baa au sehemu nyingine ambazo ni za kijamii. Epuka kutaka kukutana na mpenzi wako kwa mara ya kwanza gesti. 

Nasema hivyo kwakuwa, kama wewe ni mwanaume mpenzi wako atafikiria kwamba lengo lako si kuanzisha uhusiano ‘siriasi’ bali una lako jambo. 

Hata kama atakuja kwakuwa anakupenda lakini yawezekana akaanza kujenga picha tofauti na wewe na anaweza kukosa uhuru mtakapokuwa pamoja.

Hivyo, chagua sehemu ambayo mtakaa huku kila mmoja akijisikia huru bila kujenga mawazo tofauti kwa mwenzake.

Usiri na usalama wa eneo mnalokutana

Kikubwa cha kuangalia katika sehemu ambayo mnatarajia kukutana kwa mara ya kwanza ni ile ambayo mtaongea mambo yenu bila watu wengine kusikia wala kuwavuruga. Kama ni ufukweni, nendeni sehemu ya peke yenu lakini pia ambayo ni salama.


Msiende sehemu ambayo unahisi mpenzi wako anaweza kushindwa kuwa huru kutokana na watu kujazana au sehemu ambayo inatishia usalama wenu. Angalieni sehemu nyingine.

DOWNLOAD APP YETU GOOGLE PLAY BONYEZA HAPA

DOWNLOAD APP YETU GOOGLE PLAY BONYEZA HAPA