MAMBO 5 YA KUZINGATIA KAMA UNAUNGANISHWA NA MWANAUME USIYEMJUA

!

Inaweza kuwa ni Kanisani labda huyo mwanaume kapirtia kwa mchungaji kuwa anakutaka wewe, ni msikitini, labda kuna shehe kamfuata Baba yako kuwa kuna mtu kakupenda. Inaweza kuwa ni shoga yako, Mama yako, au dada yako, mtu unayemheshimu anakuja na kukuambia kuwa kuna Kaka anakupenda na anataka kukuoa. Ndoa ni jambo jema ila kabla ya kuona na mwanaume ambaye humjui zingatia mambo haya.

(1) Achana na stori za kusikitisha kuhusu huyo Mwanaume na chunguza kwanza; Wengi ya wanaume wanaounganishwa wanakuja na stori nzuri, mara huyu Kaka kaumizwa sana, mara huyu kaka alikua na mwanamke kamuacha na watoto, mara anataka kuoa, ni mstaarabu, umekutanishwa kanisani unasikia ni mchamungu, Shehe anakuja anakuambia ni muumini mzuri, basi dada yangu kabla ua kukubali chunguza.

Acha kuamini kila kitu unachoambiwa hata kama umeambiwa na mchungaji au shehe, umeambiwa na mtu unayemuamini, dada yako au shoga yako. Kuna baadhi ya wanaume huficha tabia zao kwa kutafuta wtau unaowaheshimu ili uwaamini sana. Lakini pia hata hao wanaokuja kwako wanaweza kuwa ni waongo, wanamtetea tu, tena kama unaunganishwa na ndugu yake kuwa makini zaidi. kwa kifupi ukiletewa mwanaume, mchunguze wewe kwanza na usisikilize ya watu.

(2) Usikimbilie ndoa jipe muda wa kuwa naye kwenye mahusiano hata kama analazimishia ndoa; Anataka ndoa lakini mchunguze kwanza, kwanini anaharaka hivyo, anaficha nini? Lakini ni mwanaume tu je unajua tabia zake, je utaweza kuzivumilia? Kua naye kwenye mahusiano, sio wiki tu mshaanza kutambulishana, anaanza hataki tendo la ndoa anataka ndoa tu lakini ndoa si tendo la ndoa tu.

Hapa ndiyo wanawake wengi mnachanganyikiwa, mwanaume akikumabia sitaki kukutumia nataka ndoa mnadhani mmepata malaika, kuna ambao hawtaaki mahusiano kwakua wana hasira, wanapiga sana, kuna ambao hatwataki tendo kwakua hata kufanya tendo kwenyewe hawawezi, kuna wengine wanaharakisha kwakua wanaona una pesa na mambo yao yamekua magumu, kuna sababu nyingi, mchunguze, kaa mahusiano hata miezi mitatu kabla ya kuingia huko kwenye ndoa, ingia ukishakua umemjua.

(3) Kama ametoka kuachwa kwa maumivu sana, usiingie kwenye ndoa ya harakaharaka analipa kisasi; Kuna wale wanaume ambao anakuambia katoka kuachwa na mke wake, mpenzi wake, unasikia stori kaumizwa sana na mtu wake hivyo alikua anaomboleza kiasi kwamba ndugu zake wakaamua kumtafutia mwanamke ambaye ndiyo wewe. Wengi unakuta wanaingia kwenye mahusiano ili kumsahau X wake, anakutumia akikusahau ndiyo basi.

Wengi akili zinakua hazijakaa sawa, mwingine unakuta anataka kumkomoa X wake, kumuonyesha kuwa na mimi naweza kupata mtu, hasa unakuta X wake kaolewa basi anachanganyikiwa na kutaka kuoa harakaharaka. Mwingine kaachwa kwa aibu, labda alishatambulisha mwanamke, wakaanza mipango ya ndoa lakini ghafla akaachwa, anataka kuoa kwakua ana maumivu, ndugu yangu, muache apone kwanza kabla ya kuingia naye kwenye ndoa.

(4) Usimtambulishe kwenu kabla hajakutambulisha kwao, haklikisha unajua kwao na usifanye mambo kwa kificho; Wanakua na kasi sana ya kuja kwenu, kutaka kukuoa, wengine unakuta anataka kukuoa kwa kificho, labda hataki watu wengi wajue, tena kama ni ndoa ya kiislamu hata kwao hakupeleki, anafanya kufichaficha. Hapana, kabla hajaja kwenu muambie akupeleke kwao, kwanza wakukubali lakini pili ufahamu kuwa ni familia ya aina gani.

Najua kuna makabila ambayo mwanamke haendi ukweni lakini angalau jua anapoishi mwanaume, usiolerwe wakati hujui hata anaishi wapi. kuna uongo mwingi, unakuta mtu kaacha mke kwao kaja mjini kaona una pesa, mnasali pamoja anasikia unataka mume anaamua kujitoa kwako ili kufaidika, hivyo akupeleke kwao, au kwake, mjue kidogo kabla ya kuingia naye kwenye ndoa.

(5) Kama una kipato kikubwa usomkaribishe kabisa kwenye mali zako, kuwa mbinafsi nazo na hakikisha anakuoa si wewe unamuoa; Wadada wengi wakishakua na pesa wanachanganyikiwa hasa wakifiksiha miaka 28 bila ndoa, yaani wanajiona kama hawataolewa hivyo wanakua na kihoro cha ndoa mpaka kila mtu anaona. Sasa kama una kipato chako, anakuja mwanaume anaongelea ndoa tu kila dakika, anakuja na maushauri mengi ya Biashara na vitu vingi basi tulia kwanza.

Acha kumuonyesha mali zako, kumuambia kuhusu pesa zako, hata kama ana kazi yake lakini kama unaona anazizungumzia mali zako sana, anaongelea kuhusu kuchanganya mali na kufanya vitu kwa pamoja punguza kasi, usimuambie sitaki kwaajili ya mali bali acha kumpa pesa na kumuonyesha pesa zako. Akuoe wewe, yaani hata kama anaishi chumba kimoja ila mnapopanga kuishi ongelea kuhusu kuishi kwake au kutafuta sehemu ya kuishi pamoja na si kupapatikia kumpa mali kwakua tu kadai ndoa.

(6) Mwisho hakuna kanunu yoyote katika kuanzisha mahusiano, mshirikishe Mungu kwa imani yako; Nilichoandika hapa ni kukutahadharisha kabla ya kuingia kichwa kichwa, mshirikishe Mungu kwa kila kitu lakini kumbuka Mungu kakupa akili, kabla ya kumuomba zitumie. Najua una hamu ya ndoa ila chunguza, hata kama unakaa kwenye mahusiano kwa wiki moja tu lakini hakikisha unamjua bizuri, ingia kwa akili zako na si kwa ahadi zake au wale waliokuunganisha.

DOWNLOAD APP YETU GOOGLE PLAY BONYEZA HAPA

DOWNLOAD APP YETU GOOGLE PLAY BONYEZA HAPA