WANAUME USALITI NI SUMU MBAYA KWENYE MAHUSIANO.
Hakuna mtu anayependa kuchangia penzi na mtu mwingine. Si mwanaume wala mwanamke.
Hakuna anayetaka penzi lake ligawanyishwe kwa mtu mwingine. Kama ndivyo, kwa nini baadhi ya wanaume mnawasaliti wapenzi wenu?
Kwa nini mnawaumiza wapenzi wenu ambao mmewatafuta na kuwagharamikia vitu vingi, ikiwemo muda, mali na vinginevyo?
Wanawake wanajiuliza, hivi ni kitu gani mwanaume unakosa kwa mpenzi wako kiasi cha kuamua kumsaliti mtu anayekupenda?
Mapenzi yanauma sana, ila usaliti unauma zaidi, ni doa na sumu mbaya sana kwenye uhusiano. Bila shaka hakuna mtu anayependa utamu wake uonjwe na mtu mwingine ndiyo maana kila siku tunasikia, wapenzi wameuana, mpenzi ameua, amefungwa, amefumaniwa, amepigwa na mambo mengine mengi, kisa kupinga kuonjwa kwa utamu wa mtu.
Mwanamke au mwanaume ambaye hana tabia za kuchepuka, mvumilivu, mwenye upendo kwa mwenza wake, siku akibaini kuwa mpenzi wake anamsaliti, moyo wake hupoteza upendo wa zamani aliokuwa nao.
Usaliti huohuo husababisha amani kutoweka ndani ya nyumba, kwa sababu mwanamke au mwanaume anafahamu kabisa kuwa mpenzi wake anam’cheat’ lakini yeye anakataa katakata.
Kinachofuatia ni mwanamke kutokuwa na imani na mumewe au mpenzi wake, hata kama akiaga kiukweli kuwa anakwenda msibani, basi mwanamke atahisi tu kuwa anakwenda kuchepuka. Hii ni hatari sana.
Ninaposema ni doa na sumu katika mapenzi, namaanisha uchepukaji au usaliti husababisha kutoweka kwa uaminifu baina ya wapenzi. Kila mmoja huwa hana imani na mwenzake. Mtindo huo husababisha kuzalisha.
Usaliti ukiendelea, huzalisha chuki baina ya mtu na mpenzi wake. Mwanamke huwa haoni tena thamani ya kumuandalia chakula mezani mpenzi wake kwa sababu anajua ni kama dharau, yaani atoke kwa mwanamke mwingine halafu yeye ndiye amuandalie chakula? Haiwezekani!