JINSI NILIVYOHANGAIKA KUPATA WAZO LA BIASHARA KIJIJINI!
Kaka naamini utakua unanikumbuka, mimi ni yule dada ambaye nilikuambia niko kijijini sana na hakuna kitu cha kufanya. Tuliongea sana kutafuta Biashara lakini kila Biashara tuliyokua tukitafuta ilikua inagoma. Mwaka jana ukaniambia kwahiyo sehemu hembu nifungue duka la kila kitu, lisiwe la vyakula ila la vitu vidogo vidogo kama cheni, makasha ya simu, midoli midole, viredio vidogo na vitu vingine vingine kama vile vya wamachinga.
Kweli Kaka nilifungua kwani kwa mazingira ya hapa vitu ni mpaka mjini, nilitafuta kijana na kumuweka na kwakua kila siku ya Jumatano na alhamisi kunakua na soko basi katika siku hizo alikua anachukua badhi ya vitu anapeleka. Mimi ni mwalimu hivyo siku Jumatano na Alhamisi alikua anaenda yeye ila siku ya Jumamosi tulikua tunaenda pamoja.
Nimefanya hii kazi kwa karibu mwaka sasa nashukuru kukuambia Kaka kuwa nimefanikiwa, sasa hivi nina duka kubwa tu na niseme si kubwa kihivyo ila vitu vinatoka. Bado hapajachangamka sana ila angalau napata na kikubwa kinachoniingizia ni mnadani. Nimemchukua kijana wa hukuhuku na nimebahatisha anayejua Biashara, watu wa huku wana ukabila akikaa mtu wa kwao angalau ananunua, nashukuru sana kwa kuniamsha!