NDOTO UNAZOLETEWA NENO & NDOTO AMBAZO JINA LA MTU NDIO LIMEBEBA UJUMBE.
A. NDOTO UNAZOLETEWA NENO:
“Basi nililetewa neno kwa siri, Sikio langu nikasikia manong’ono yake. Katika mawazo yaliyotoka katika maono ya usiku, Hapo usingizi mzito uwaangukiapo wanadamu” (Ayubu 4:12—13).
Hizi ni ndoto ambazo naamini kila mtu anayeota ndoto amewahi kuziota. Kila neno unaloletewa ndotoni, chimbuko lake ni Mungu, Shetani, au wewe mwenyewe. Kuna njia kadhaa ambazo unaweza kupewa neno:
1. Neno unalolisikia: Ukiwa ndotoni, unaweza kusikia watu wakiongea, au ukasikia sauti lakini usione mtu.
Neno linasema, “Hata alipofariki Herode, tazama, malaika wa Bwana alimtokea Yusufu katika ndoto huko Misri, akasema, Ondoka, umchukue mtoto na mamaye, ushike njia kwenda nchi ya Israeli; kwa maana wamekufa walioitafuta roho ya mtoto” (Mathayo 2:19—20).
Hii ni njia ambayo Mungu na Shetani wanaweza kuitumia kuleta neno kwa mtu. Mungu anaweza kutumia malaika au njia nyingine ili kukufikishia ujumbe.
Kumbuka unaweza kuona malaika ndotoni na wakaonekana kama watu (Waebrania 13:2).
Ukisikia sauti ndotoni, tumia kipimo cha neno la Mungu kujua chanzo chake na kusudi lake. Shetani anaweza kuleta neno ndotoni kwa kusudi la kujaribu kuuwa vitu fulani (Ayubu 4:12—17).
Kuna mtu mmoja aliota ndoto kuwa amepewa simu ya mtumishi fulani. Halafu baada ya kuichukua ile simu na kuweka sikioni, akaanza kusikia sauti ya mtu fulani ambaye amekwisha kufariki.
2. Neno unalopewa useme kwa kinywa chako: Kuna wakati ukiwa ndotoni unasema maneno fulani halafu ukiamka, unaweza kushangaa kwa nini ulikuwa unazungumza maneno uliyosema.
Namjua mtu ambaye alikuwa amelala na mke wake na nguvu za Mungu zilimshukia akiwa amelala na akaanza kusema “Mimi ni Mungu wa Ibrahimu” na akaanza kutabiri.
Cha ajabu ni kwamba, mke wake alimsikia akinena kwa lugha ila yeye alielewa kila kitu kwani alikuwa akizungumza lugha ya Kiswahili. Hii inatokea kwani Mungu anatumia lugha yake kusema nasi ila Roho Mtakatifu ndiye anayetafsiri kulingana na lugha tunayoielewa.
Hivyo Mungu anaweza kutia neno kinywani mwako kama alivyofanya kwa Yeremia. “Ndipo BWANA akauonyosha mkono wake, akanigusa kinywa changu; BWANA akaniambia, Tazama, nimetia maneno yangu kinywani mwako” (Yeremia 1:9).
Kama Mungu ametia neno ndani ya kinywa chako na ndani ya ndoto ukaanza kusema maneno fulani, jitahidi uyaandike mahali kwani hapo ni Mungu anakuwa anaongea kupitia wewe.
Hivyo maneno ambayo unayaongea ndotoni ni ya muhimu na yanaweza kuwa yanakuambia siri zilizopo rohoni mwako ambazo yamkini huzijui kwa jinsi ya mwili.
Neno linasema, “Maana ni nani katika binadamu ayajuaye mambo ya binadamu ila roho ya binadamu ili ndani yake? Vivyo hivyo na mambo ya Mungu hakuna ayafahamuye ila Roho wa Mungu” (1 Wakorintho 2:11).
Binafsi ni mara nyingi naota nikiwa najifundisha neno la Mungu na najua Mungu anaweka maneno kinywani mwangu ili kunifundisha kile anachotaka nikifahamu.
Lakini pia Shetani anaweza kutia maneno ndani ya mtu kama alivyofanya kwa Petro (Mathayo 16:22—23). Unachohitaji ni kuomba Mungu akusaidie kutofautisha neno la Mungu na neno la Shetani. Neno la Mungu wakati wote litaambatana na maandiko.
3. Neno unalopewa kwa njia ya maandishi: Wakati mwingine, unaweza kupewa neno kwa njia ya maandishi. Mungu anapokuletea neno kwa njia ya maandishi, hatumii lugha za duniani bali anatumia lugha yake.
Belshaza alipewa neno na Mungu kwa njia ya maandishi “MENE, MENE, TEKELI, NA PERESI” (Danieli 5:25).
Kuna wakati unaweza kupewa neno kwa njia ya maandishi. Kama ni ujumbe kutoka kwa Mungu, atatumia lugha yake na Roho Mtakatifu anatafsiri na wewe unaona maandishi kwa lugha yako.
Wakati mwingine, unaweza kupewa neno usilielewe na wala usilione kwenye kamusi. Kinachotakiwa ni kuingia kwenye maombi mpaka upate tafsiri yake.
Kuna njia zingine ambazo unaweza kupewa neno ndotoni. Haya ni maneno yanayolenga kukusaidia kitu fulani (kama chanzo chake ni Mungu) na kujaribu kuua kitu fulani (kama chanzo chake ni Shetani).
B. NDOTO AMBAZO JINA LA MTU NDIO LIMEBEBA UJUMBE
Ukiacha ndoto ambazo unaonyeshwa watu waliokufa, kuna ndoto ambazo unaona watu fulani na wakati mwingine, unakuwa unaongea nao.
Hawa ni watu ambao unakuwa unawafahamu kwa jinsi ya mwili na wanaweza kuwa ndugu zako, rafiki zako, au watu unaoishi nao. Ndoto hizi huwa zinakuwa na ujumbe katika maeneo fulani.
Leo tuangalie maeneo kama matano:
1. UJUMBE ULIOPO KWENYE JINA:
Mungu anapokuwa anasema nasi kupitia ndoto, anatumia mazingira ambayo sisi tunaweza kuyaelewa. Hivyo kuna ndoto ambazo unaweza kuziota na ujumbe wa ndoto ukawa kwenye jina la mtu unalopewa ndotoni.
Kwa mfano maandiko yanasema, “Nikaona, na tazama, farasi wa rangi ya kijivujivu, na yeye aliyempanda jina lake ni Mauti, na Kuzimu akafuatana naye” (Ufunuo 6:8a).
Katika maandiko haya, ujumbe haupo kwenye aliyempanda farasi bali kwenye “jina la aliyempanda.” Hata katika ndoto, ni hivyo hivyo.
Usiku mmoja niliomba Mungu anisaidie na kunipa kitu cha kufundisha. Usiku huo, niliota ndoto niko na mtu ambaye nilisoma naye sekondari halafu nikawa namwambia maandiko katika kitabu cha Ufunuo.
Baada ya kuamka, nilielewa yale maandiko lakini sikuelewa kwa nini nilikuwa na huyo mtu kwani sikuona uhusiano wowote. Ndipo Roho Mtakatifu akanifunulia kuwa “ujumbe” upo kwenye jina.
Lilikuwa jina la kinyakyusa hivyo nikauliza maana ya jina nikaambiwa “Msaidizi.” Nikaelewa uhusiano wa hiyo ndoto na kile Roho Mtakatifu alikuwa anafanya kama Msaidizi wetu (Yohana 14:26).
Hivyo kuna ndoto ambayo unaweza kuiota lakini ujumbe unakuwa kwenye jina la yule unayemuona ndotoni. Nikupe mfano mwingine:
Wakati naandika kitabu cha ndoto cha English, siku moja niliota nipo na mtu mmoja anaitwa “Simon” ambaye tulisoma naye sekondari. Alikuwa anaongea nami lakini aliyokuwa anayaongea yalikuwa hayaeleweki.
Usiku huo huo, nikajikuta niko mazingira mengine tofauti na mtu mwingine ambaye tulisoma naye sekondari na jina lake naye ni Simoni. Ndoto ya pili ilikuwa tofauti kabisa na ya kwanza.
Nilipoamka, nilizitafakari hizo ndoto na nikajua kuwa ujumbe uko kwenye jina ila sikuchukua hatua yoyote. Usiku uliofuata, nikaota ndoto nyingine niko huku Marekani na mtu ninayemfahamu wa huku, naye jina lake ni Simon.
Baada ya hapo, nikafahamu hakika kuwa kwenye kitabu cha English nilichokuwa ninakiandika, mahali ambapo kuna jina la Simon, kuna kitu natakiwa kubadilisha.
Niliangalia kitabu nilichokuwa nakiandika nikaona kuna kosa fulani katika ndoto iliyoambatana na maandiko haya: “Simoni Petro akamwambia, Bwana, si miguu yang utu, hata na mikono yangu na kichwa changu pia” (Yohana 13:9).
Siku nyingine niliwahi kuota ndoto fulani halafu nikamuona mtu anayeitwa Andrew akifuatana na kaka yangu anayeitwa Peter na mimi nikafuata.
Niliposhtuka, nilielewa kuwa ujumbe upo kwenye majina kwani hapo kulikuwa na Andrea, Petro, na Yakobo (majina ya mitume wa kwanza Yesu aliowaita) (Mathayo 4:18—21).
Hivyo kuna ndoto ambazo unaweza kuziota na ujumbe ambao Mungu anataka uupate ukawa kwenye jina la mtu unayeoneshwa na siyo kwenye tukio.
Ili uweze kutambua ndoto ambazo ujumbe uko kwenye jina, siyo tukio, mara nyingi hutaona uhusiano wowote ule kati ya mtu unayemuona na tukio unaliliona.
Ukisoma Biblia, utaona kuwa watu wengi walikuwa wanapewa majina kutokana na kitu fulani. Kwa mfano, kuna maandiko yanayosema:
“Nakusihi, bwana wangu, wewe usimwangalie huyu mtu asiyefaa, yaani, Nabali; kwa maana kama lilivyo jina lake ndivyo alivyo yeye; jina lake ndilo Nabali, na upumbavu anao;” (1 Samueli 25:25 a,b).
Pia tunaona watu kama Yakobo aliyepewa jina la Israeli, Abramu aliyepewa jina la Ibrahimu na wengine wengi.
Mungu anaposema nasi kupitia ndoto, anaweza kabisa kukuonyesha mtu unayemfahamu lakini ujumbe ukawa kwenye jina la unayemuona. Utafahamu pale ambapo ujumbe upo kwenye jina ikiwa uhusiano wa ndoto unayoota na tukio havihusiani.
Lakini pia kama ukipewa ndoto zenye watu tofauti ila majina yanafanana, unajua kuwa ujumbe upo kwenye jina.
Mfano: Siku moja nilikuwa natakiwa nifundishe neno la Mungu mahali fulani na usiku huo niliota nipo nafundisha neno la Mungu na mtu mmoja anayeitwa Immanueli tuliyesoma naye shule ya msingi amesimama pembeni yangu madhabahuni.
Nilielewa ujumbe upo kwenye jina la Immanuel, yaani Mungu pamoja nasi (Isaya 7:14 & Mathayo 1:23).
Siku nyingine niliota nipo na mke wangu halafu akatokea mtu anayeitwa Immanuel akamchukua wakawa wakiondoka nami nilikuwa na amani moyoni.
Baada ya ndoto hiyo, nikaota ndoto nyingine nikamuona askofu fulani ameenda nyumbani kwa mtu anayeitwa Immanuel na kumchukua mke wake wakaondoka naye. Nikawa nasikikitika kumuona huyo askofu alichofanya.
Niliposhtuka nilielewa kuwa ujumbe upo kwenye jina la “Immanueli.” Mke wangu kuambatana na mtu anayeitwa Immanueli tafsiri yake ni kwamba kanisa linatakiwa liambatane na Kristo kwani yeye ndiye kichwa cha Kanisa. Paulo alieleza siri ya kanisa la Kristo kwa kutumia mke na mme (Waefeso 5:23—33).
Lakini pia kuonyeshwa askofu fulani ameenda kumchukua mke wa mtu anayeitwa Immanueli nami kusikitika ilikuwa inatupa ujumbe kuwa “dini ndiyo inayopotosha kanisa la Kristo.”
Siku moja mtu mmoja aliota ndoto akiulizwa “nikupe Ibrahimu” akasema “Yes Lord.” Akaambia akasome Mwanzo 15 (habari ya jinsi Mungu alivyomtokea Ibrahimu). Siku nyingine akaota ndoto yuko na mtu anaiyeitwa Ibrahimu akimfundisha juu ya Roho Mtakatifu.
Kuna mifano mingi naweza kukupa ambayo ujumbe wa ndoto unakuwa kwenye jina la mtu unayeonyeshwa. Hizi ni ndoto ambazo wakati mwingine zinajirudia na unaonyeshwa watu tofauti ila wenye jina linalofanana.
Ukiota hizi ndoto, tumia muda kuziombea ili uweze kujua ujumbe ambao Mungu anaokupa.
2. UJUMBE ULIOPO KWENYE MTU:
Hizi ni ndoto ambazo naamini kila mtu huwa anaziota. Unaweza kuwa unaombea jambo fulani, na Mungu akakuletea picha ya mhusika mwenyewe.
Kuna mtu alitujulisha juu ya mtu ambaye amewahi kumuota zaidi ya mara 30 katika matukio tofauti. Ndoto kama hizi zinakuambia kuwa kuna mambo ya kiroho yanayoendelea kwa huyo mtu na kuna uhusiano na hali ya maisha uliyonayo.
Neno linasema, “Niite, nami nitakuitikia, nami nitakuonyesha mambo makubwa, magumu usiyoyajua” (Yeremia 33:3).
Kuna mambo ambayo hatuyajui kwa jinsi ya mwili lakini Mungu anayajua na tukijiachilia kwake anaweza kutuonyesha ili kutusaidia. Hivyo kuna ndoto zingine ambazo unaonyeshwa watu fulani na ujumbe unakuwa juu ya huyo mtu unayemuona.
MFANO 1: Kuna ndoto mpendwa aliiota. Aliota watu kama wanaogelea kwenye maji mikono yao wameinyosha juu wima kabisa. Wakatoka majini na wavu ambao ulikuwa na simba, na wale simba wakaja katika nchi.
Wale simba walikuwa na sura kama ya mwanadamu. Basi yule mtu akakimbia akaingia kwenye nyumba moja ambayo haijaisha ukuta na ukuta ni mfupi kweli. Baadae akawaona watumishi wawili wakubwa Tanzania wameshika Biblia.
Lakini zile Biblia, walikuwa wamezishika kwa kuzigeuza juu ndio pako chini na chini pako juu. Mtumishi mmoja kati ya hao wawili alikuwa pia amesokota nywele zale na hazipo kama zilivyo.
Akawaambia wale watumishi “ili hao simba wasiwavamie, inatakiwa mshike Biblia sawa.” Akachukua Biblia ya mtumishi mmoja na kumuonyesha jinsi ambavyo anatakiwa kuishika hiyo Biblia. Amemaliza tu kuwaonyesha, akashtuka ndotoni.
Hii ni ndoto ambayo unaweza kuona kabisa ujumbe ulikuwa ni juu ya hao watumishi wawili na jinsi ambavyo hawatumii neno la Mungu sawasawa na Mungu alivyokusudia. Ndio maana walikuwa wameshika Biblia kwa kugeuza.
MFANO 2: Kuna mtu mmoja aliota ndoto ya ajabu. Alikuwa na dada mmoja halafu walikuwa eti wanakimbizwa na Shetani. Wakaenda na kujificha mahali fulani. Sasa yule dada aliyekuwa naye akaanza kupumua kwa haraka sana kwa kuogopa.
Mwenzie akasema moyoni “kwa upumuaji huu, Shetani atatupata.” Basi akamshika mwenzie mkono na kuanza kukimbia. Yule Shetani aliwakimbiza halafu akabadilika uso na kuwa nabii mmoja mkubwa sana Africa.
Baadae wakaruka ukuta ila yule nabii akashindwa kuruka akazunguka. Yule mtu akaanza kuomba kwa kunena kwa lugha na yule nabii naye anaomba kwa lugha. Yule mtu akamwambia yule nabii “muda si mrefu watu watagundua kuwa kunena kwako kwa lugha hakutokani na Mungu.” Baada ya hapo akashtuka.
Kama week moja baadae, nami nikaota nipo napambana na huyo nabii halafu mimi nikawa nikinena kwa lugha na yeye ananena kwa lugha. Alikuwa akitoa nguvu katika mikono kujaribu kuniangusha, mimi nikawa nazizuia.
Mwisho nilifanikiwa kumfunga kabisa halafu nikamwambia “naenda kuwaita wafuasi wako ili wakujue wewe ni nani.” Baada ya hapo nikashtuka ndotoni. Nilielewa kuwa ujumbe unahusu huyo nabii wa uongo anayedanganya wengi.
Hivyo kuna ndoto ambazo Mungu anakufunulia siri za rohoni juu ya mtu fulani.
Unapokuwa unaoota ndoto hizi, muombe Mungu akusaidie kutofautisha juu ya ndoto ipi ni ya Mungu na ipi ni ya Shetani kwani neno linasema, Shetani anaweza pia kujigeuza kama malaika wa nuru (2 Wakorintho 11:14).
Ila unapoota sana juu ya mtu fulani na ndoto ikawa inajirudia kwa namna tofauti, maana yake kuna kitu cha kiroho ambacho Mungu anataka ufahamu juu ya huyo mtu. Ndio maana tunatakiwa wakati wote tutafsiri vitu kwa jinsi ya rohoni.
Yesu alionya kuwa “Si kila mtu aniambiaye, Bwana, Bwana, atakayeingia katika ufalme wa mbinguni; bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu alite mbinguni” (Mathayo 7:21).
Usiweke imani kwa mtu kwa sababu tu anaonekana ni mtumishi kwani Yesu alisema watakuja wamevaa mavazi ya kondoo walakini kwa ndani ni mbwa—mwitu wakali (Mathayo 7:15).
Kwa sababu Shetani anafahamu hili, mara nyingi atafumba watu macho ili wasiweze kuona kuwa wanadanganywa.
Unaona malaika alikuja kumletea Danieli majibu na neno linasema mfalme wa uajemi alipambana naye kwa siku 21 mpaka Mikaeli, malaika mkuu, akaja kumsaidia (Danieli 10:12—13).
Kuna ndoto ambazo Mungu anakusudia kukufunulia macho ya rohoni ili uweze kuona vitu na kusimama katika kweli ya Mungu, lakini Shetani atahakikisha unafumbwa macho.
Kwenye kitabu cha ndoto, niliandika jinsi ambavyo malaika wa Mungu au Shetani wanaweza kuwatokea watu kupitia ndoto. Kama jinsi ambavyo malaika wa Mungu wanaweza kukutokea kwa sura ya mwanadamu, malaika wa Shetani nao wanaweza kukutokea kama watu.
Hivyo kuna watu wengine ambao unaweza kuwa unaonyeshwa ndotoni lakini ni roho zihudumiazo (Waebrania 1:14).
MUHIMU: Kitu kikubwa na cha muhimu ni kusimama katika neno la Mungu na kuishika kweli yake na Mungu atakufunulia yanayoendelea katika ulimwengu wa roho.
Kama unahitaji kujifunza zaidi masomo ya ndoto, unaweza kupata nakala ya kitabu cha ndoto.
Mungu akubariki,
Jacob