KAMA HUWEZI KUDUNDULIZA MSHAHARA WAKO BASI JUA HATA MKOPO UTAULA!
Dada mmoja alinifuata kuniomba ushauri, yeye ni mfanyakazi serikalini, aliniambia anataka kuchukua mkopo ili kuanzisha biashara, baada ya kumsikiliza sana nilimuambia asichukue mkopo bali adundulize mtaji kidogo, nikamfundisha namna ya kuanza biashara yake bila kuchukua mkopo. Akaniambia Kaka mshahara wangu ni mdogo hivyo siwezi kudunduliza, nilimuuliza sasa anategemea nini akichukua mkopo, si ndiyo mshahara utapungua zaidi.
Akasema atakua anakula faida ya biashara, nilimuambia hapana, ukichukua mkopo utaula biashara hurafungua na utaishia kukatwa tu kila siku. Aliniuliza kwanini mbona namkatisha tamaa? Nikamuambia sio kama namkatisha tamaa bali ndiyo ukweli. Nikamuambia kuwa mahesabu ambayo anayapiga kuhusu biashara ni ya kusadikika, katika makaratasi, hakuna hiyo faida anayoiamini, pili nikuwa mshahara wake kwa sasa hautoshi.
Nilimuambia kama kwa sasa unapokea laki tano, hazitoshi huwezi kudunduliza, ukichukua mkopo utaanza kukatwa na utakua ukipokea laki mbili. Hii inaana kuwa hazitatosha kwa matumizi yako. Utahitaji kitu kingine cha ziada ili kujazia kile kilichobakia, lakini htakipata kwakua si kama ajira kwamba unaanza leo na baada ya mwezi unaanza kulipwa, hapana, biashara inaweza kuanzas kulipa hata baada ya mwaka mmoja.
Nikamuambia labda kama una mpango wa kudanga lakini kama utategemea biashara ikupe faida ya kujazia ile laki tatu kwa mwezi basi sahau kuwa inawezekana kwa mipango yako hiyo. Aliona kama namkatisha tamaa na kuchukua mkopo, lakini bada ya miezi mitatu alinipigia simu, bado hajaanza biashara kwani kila anayojaribu anashindwa namna ya kuanza na mkopo anakatwa na ashaanza kula mkopo wenyewe hajui chakufanya.
Baada ya kumsikiliza niliona kuwa atakula mtaji, nilimshauri kununua Bodaboda kabla pesa hazijaisha ili angalau awe na kitu cha kumuingizia kipato. Alinunua pamoja na kwamba inamsumbua kila siku lakini angalau ana kitu cha kujazia ile laki tatu na angalau hali tena ule mtaji wake ambao ameukopea. Ndiyo unaweza kukopa na kufanikiwa lakini hakikisha una mipango mizuri na hicho unachotegemea kukifanya angalau unakijua na si kukurupuka kutafuta pesa ya haraka.