SIMULIZI FUPI: USIKU WA KIFO CHANGU.

MWANDISHI: SADARI KISESA.
SIMULIZI FUPI: USIKU WA KIFO CHANGU.

ANZA NAYO...
“Alitamani utajiri akaja akaupata utajiri, alijua akiwa tajiri atakuwa na furaha na kila akitakacho hapa duniani atakipata kwa pesa alizokuwa nazo. Akujua kuwa utajiri una changamoto na majuto yake, aliendelea kuwa na maisha yake ya utajiri bila hata kujua kweli utajiri ungempa furaha au kilio na mateso mpaka uhai wake utakapofika tamati. Alijiona maisha kayapatia haswaa ilifika kipindi akawa anatembea kwa mwendo wa madaha akiringia huo utajiri aliokuwa nao, alikuwa si mtu mwengine bali alikuwa ni Fetu binti Suruku. Fetu alikuwa ni mwanamke mrembo ambaye aliyechukizwa na mkorogo, weupe wake ulikuwa si wa kujichubua ni alikuwa mwenye umbo namba nane tena mwenye kuvutia kila mwanaume aliyemtazama umbo lake kwa uweredi. Fetu licha ya kuwa na madaha ya kuringia utajiri wake pia alikuwa na madaha ya kuringia ulimbwende wake, maisha yake ya kuishi Masaki mkabala na barabara kuu kwenye nyumba ya ghorofa moja ya kifahari iliyozungushiwa uzio lenye geti jeusi lilobandikwa picha ya Mbwa mwitu na chini ya picha ile ikinakshiwa kwa maneno mekundu yasemayo:- “Nyumba hii kuna Mbwa mwitu mkali tafadhali usijaribu kupita eneo hili wakati wa usiku.”, yalisonga hatimaye alipomaliza miaka miwili tu. Usiku pembezoni mwa nyumba yake kulikuwa na makaburi yapatayo matatu moja lilikuwa ni kaburi la mtoto wake kipenzi ambaye aliyekufa kwa ajali ya moto katika kipindi cha nyuma kidogo, kaburi la pili lilikuwa ni kaburi la mama yake mzazi ambaye aliyekufa kwa mshtuko wa moyo katika kipindi cha awali na kaburi la tatu lilikuwa ni la mumewe ambaye alikufa kwa kujinyonga kipindi cha nyuma wakati anapitia changamoto za maisha. Kaburi la mumewe kwenye msalaba kuliandikwa jina ambalo lililofahamika kwa majina ya Soloko Dikina.... Kaburi lile usiku wa siku ya Jumatano lilionekana kujengeka nyufa mwishowe likapasua katikati kisha alionekana kutokea mtu mrefu kiasi, aliyevalia sanda nyeupe na macho yake kung'ara mfano wa Paka, Chui hama Simba. Mtu yule alitokea eneo lile kwa sura ngeni hakufanana na Soloko alikuja duniani kwa sura isiyotambulika na inayotisha kwa kila mtu aitazamapo, mtu yule kwa kumtazama kwa uweredi alikuwa ni mzimu. Mzimu ule kwa mwendo wa polepole moja kwa moja ulielekea mpaka kwenye geti la kuingilia ndani kwa Fetu. Hapo ulikutana na Mbwa mwitu ambaye kwa wakati ule alikuwa kashafunguliwa sasa analandalanda eneo lile la pale nje kwaajili ya ulinzi ambao windo la kila siku, ulipoonana ana kwa ana na Mbwa yule papohapo alibwekewa na yule Mbwa mwitu. Ingekuwa ni binadamu wa kawaida kwa kubwekewa na Mbwa mwitu yule haki angetoa nduki, lakini kwakuwa ni mzimu hivyo hakumwogopa Mbwa mwitu wala hakuogopa usiku ule mnene. Yeye aliyayuka akatokea kwenye sebule ya kifahari ya Fetu huku nje alimwacha Mbwa mwitu akizidi kubweka na kuendelea kuzunguka kila pahala kwaajili ya kumtafuta yeye aliyemtia machoni hivi punde tu, alipoingia ndani mzimu ulibadilisha hali ya hewa yote. Manukato yaliyokuwa yakinukia katika nyumba ile yalizizima hayakusikika tena kwasababu ya harufu ya uozo iliyosikika pindi tu ulipowasili mzimu, sebule yote aliyokuwepo yeye ilibadilika ilinuka kama mzoga ulioanza kutoa funza. Yaani kwa harufu ile mbaya iliyokuwa imeenea nyumba nzima kwa binadamu wa kawaida asingeweza kustaimili, Fetu sababu alizoea harufu ile na alikuwa kashajua ile harufu inatokana na kiumbe gani basi pindi alivyoshtuka kitandani na kuamka hakustaajabu bali alitoka chumbani kwake alielekea mbio sebuleni inapotokea harufu ile akiwa mwenye sura ya furaha iliyojenga tabasamu mwanana kana kwamba ugeni ule ni wa baraka kwake na maisha yake ya kila siku.

“Kipenzi, waoooh!!,” Fetu alilaki kwa kukumbatia mzimu mara baada ya kufika karibu yake na mara baada ya ule mzimu kubadilika sura yake ile ya kutisha na kuwa Soloko. Fetu alipomkumbatia Soloko harufu ile ya uozo iliongezeka maradufu lakini mwenyewe hakujali kwasababu tayari kashaizoea. 

“Inaonekana ulinikumbuka sana mke wangu, maana sio kwa furaha hiyo uliyokuwa nayo,” Soloko alisema kwa sauti ya kujirudiarudia kama mwangwi huku akipalaza nywele za mkewe kwa mkono wake wa kuume uliokuwa na kucha ndefu za kung'ara mfano wa urefu wa vocha. Fetu alibaki akitabasamu huku akijaribu kumtazama mumewe kila pahala wa mwili wake mara baada ya kuacha kumbato lilopita sekunde chache za nyuma, wala akuendelea na mazungumzo tena na mumewe alimkalisha mumewe kwenye sofa la mtelezo kisha alikwenda chumbani kwake kumchukulia mumewe kinywaji. Dakika hazikupita nyingi alirudi tena sebuleni huku akiwa ameshikilia bilauri ya rangi ya kijani iliyokuwa na damu nusu ya Paka ndani yake.

“Kipenzi, karibu kunywa kinywaji chako cha kila siku ukipendacho,” Fetu alimkaribisha Soloko kile kinywaji alichokileta mara baada ya kumkabidhi mumewe mkononi, Soloko alikipokea kinywaji kile kwa taratibu huku akimkazia jicho Fetu kisha alizishikashika nywele zake nyingi ndefu za kichwani zilizotimuka shaghara baghara huku akiendelea kunywa kinywaji chake alicholetewa. Alipomaliza kunywa kile kinywaji alirudisha bilauri kwa mkewe, bilauri ikarudishwa hatimaye Fetu akarudi tena kujumuika na mumewe sebuleni lakini safari hii aliporudi alikuta mabadiliko. Alimkuta Soloko yupo tofauti na awali alikuwa anatoka funza mwili wake wote lile jambo lilimshtua na amani ya moyo ilikwisha moyoni mwake aliogopa sana kiasi kwamba hakutamani tena kumsogelea mumewe, mapigo ya moyo yalimdunda bila ya idadi akavuta pumzi ndefu ya uwoga baada ya kuona mumewe akimfuata huku akiangua kicheko cha mwangwi kilichojaa kejeli. Alijaribu kukimbia kwenda chumbani kwake cha ajabu alipofika katika mlango wake wa chumbani haukutaka kufunguka ulijifunga kwa mazingira ya kutatanisha, hofu pana ilijaa rohoni mwake usiku ule alitamani kwake upite salama lakini ikashindikana alijitahidi kupiga yowe la kuomba msaada kwa majirani lakini ilishindikana kwasababu ya sauti yake ilizuiriwa kwa mazingira ya kutatanisha isiweze kutoka nje ya nyumba ile.

“Leo ni tarehe ngapi, mwezi wa ngapi na mwaka elfu mbili na ngapi?,” Soloko aliuliza mara baada ya kusogea mpaka pahala alipokuwepo Fetu, Fetu alijaribu kuvuta kumbukumbu vema kwa kuvuta hisia usoni mwake kisha akaropoka kwa kujibu kwa uwoga uliokithiri.

“Leo ni tarehe 8, mwezi wa 10 na mwaka 2012.”

“Vizuri. Umekumbuka tarehe ya leo, mwezi wa leo na mwaka huu...tulikubalianaje?,” Fetu alivuta kumbukumbu kwa mara ya pili kisha alijibu kwa kupayuka kwa sauti kali lakini iliyoishia nyumba ileile tu.

“Lakini si ulisema utajiri wangu utakufa na mimi mwenyewe nitakufa leo, pale pindi utakapotapika kinywaji nitakachokuletea?.”

“Ndiyo. Ila unakumbuka kuwa nilikuambia usipoona nimetapika ukiona nimetokwa na Funza jua tayari uhai wako na maisha yako yashakwisha. Sikusema?.”

“Ulisema. Ila.....”

“Ila nini kipenzi kama kuponda mali ushaponda vya kutosha, lakini kwasasa naomba timiza makubaliano yetu.... Nilikupatia utajiri hapo awali kwa makubaliano, sasa leo mkataba wetu umeisha tafadhali kuwa mpole nitachukua mali zangu na uhai wako kama tulivyokubaliana huko kipindi cha nyuma,” Soloko aliyasema yale kisha alikwenda kumkumbatia Fetu pahala alipokuwepo ameganda ndi!! kama sanamu. Wasaa haukwenda sana wakiwa bado wamekumbatiana kwa huba zito ghafla Soloko alimchoma Fetu kooni na ukucha wake mrefu wa mkono wa kuume uliochongoka mfano wa mkuki na papohapo Fetu alikwenda sakafuni akaaga dunia, zilipita nusu saa Soloko aliyayuka na Fetu huku nyuma nyumba ilipotea na mali zote ambazo alizokuwa anatumia Fetu zikapotea katika mazingira ya kutatanisha.”

“Mali nzuri zile za baraka uletewazo na Mwenyezi Mungu, wala sio zile zinazohatarisha uhai wako na kuteketeza maisha yako. Naamini ukizidi kupambana kwa kila hali utajiri wa baraka lazima utapata tu, tumia akili, nguvu na karama yako uliyopewa ili uje kupata mali zisizo na mabano wala misamiati.”
                MWISHO.
Nisaidie kupenda kurasa hii itakayokuelimisha kwa simulizi mbalimbali za mafunzo kedekede 👇.
https://www.facebook.com/sadarikisesatz/

DOWNLOAD APP YETU GOOGLE PLAY BONYEZA HAPA

DOWNLOAD APP YETU GOOGLE PLAY BONYEZA HAPA